Wednesday, September 29, 2010

Utamaduni na Utandawazi


Habari hii ameichapisha Profesa Joseph L.Mbele kwenye blogu yake , nami imenigusa kiasi cha kuamua kuiweka Maisha na Mafanikio, ili habari ienee zaidi kadiri iwezekanavyo

---------------------------------------------------------------------------------------

Tangu mwaka jana, nimekuwa naendesha warsha hapa Tanzania kuhusu utamaduni na utandawazi. Mwaka jana nilifanya hivyo Arusha, na mwaka huu nimeendesha warsha Tanga na Dar es Salaam. Warsha hizi zimehudhuriwa na watu kutoka Tanzania, Kenya, Cameroon, Uingereza, Sweden, na Marekani. Hao wa nchi za nje ni watu waliokuwepo Tanzania kwa shughuli mbali mbali.

Niliamua kuanza kuendesha warsha hizi hapa Tanzania kutokana na kutambua kuwa ni muhimu katika dunia ya leo inayozidi kuwa kijiji. Watu wa tamaduni mbali mbali wanazidi kukutana kwa sababu mbali mbali, kama vile biashara, masomo, utalii, na uwekezaji. Watu wa tamaduni mbali mbali wanajikuta wakifanya kazi pamoja viwandani, maofisini, na kadhalika. Wanafunzi, watafiti, na walimu, wanajikuta wakishughulika na watu wa tamaduni mbali mbali.

Hali hii inaweza kusababisha migogoro ya aina aina, kwani kila mtu ana namna yake ya kuongea, kufikiri, kufanya mambo, ambayo inatokana na utamaduni wake. Bila kuelewa utamaduni wa wengine, matatizo lazima yatatokea, kama vile kutoelewana na kugombana.

Kwa miaka mingi katika kufundisha Marekani, nimehusika pia katika kutoa ushauri kwa waMarekani kuhusu utamaduni wa waAfrika. Wamarekani hao ni wale wanaokuja Afrika, iwe ni kwa masomo, utalii, shughuli za kidini, au za kujitolea. Nimehusika pia katika kutoa ushauri kwa waAfrika waishio Marekani, kuwasaidia kuulewa utamaduni wa Mmarekani.

Uzoefu huu umenifungua macho kuhusu umuhimu wa suala hili la kuelewa tamaduni mbali mbali, hasa kwa kuwa dunia inabadilika na kuwa kijiji. Hatutaweza kukwepa maingiliano baina ya tamaduni mbali mbali. Wafanya biashara watahitaji kutafuta masoko katika nchi za mbali, au watahitaji kutafuta washiriki kutoka nchi za mbali, au watahitaji kutafuta malighafi kutoka nchi za mbali. Makampuni yatahitaji kuwaajiri watu kufanya shughuli zake sehemu mbali mbali duniani, na katika kufanya hivyo, yatawajibika kuwaajiri watu wa tamaduni mbali mbali.

Kutokana na uzoefu huu nilioupata Marekani, niliona niko tayari kufanya warsha Tanzania. Nilikuwa na hamu ya kukutana na waTanzania na kuona nitafanikiwa vipi kuleta ujumbe wangu.

Jambo la kwanza nililofanya katika warsha hizi ni kuelezea maana ya utamaduni na maana ya utandawazi. Utamaduni, kama nilivyogusia, ni dhana inayojumlisha tabia, mwenendo, hisia na taratibu za maisha. Hata namna ya kuzungumza hutofautisha utamaduni mmoja na mwingine, kiasi kwamba, kwa mfano Mmarekani akisema jambo, linaweza kuonekana kuwa ni maudhi kwa Mwafrika au utovu wa heshima, wakati kwa utamaduni wa Mmarekani, ni usemi wa kawaida au wa heshima. Kadhalika, Mwafrika anaweza kusema jambo ambalo ni la kawaida au la heshima katika utamaduni wake, lakini likawa kero kwa Mmarekani.

Kuhusu utandawazi, dhana yangu ni kuwa utandawazi haukuanza miaka yetu hii, kama wengi wanavyofikiri. Ni jambo lililoanza zamani sana, tangu enzi za binadamu wa mwanzo kabisa. Utandawazi ulianza pale binadamu waliposambaa kutoka Afrika, ambako ndiko walikoanzia, na kuenea duniani. Kuenea huku kwa binadamu kuliandamana na kuenea kwa ujuzi, maarifa, lugha, na mambo mengine mengi.

Utandawazi ulichukua sura mbali mbali kadiri historia ilivyosonga mbele. Katika enzi zetu, utandawazi umetawaliwa na kuenea kwa ubepari, ambao umeathiri uchumi, siasa, utamaduni, na mambo mengine mengi.

Pamoja na hayo, bado tunazo tofauti za tamaduni ambazo zinaweza kuwa kipingamizi tunapokutana na watu wa nchi mbali mbali. Hapo ndipo ulipo umuhimu wa kujielimisha kuhusu tofauti hizi.

Baada ya kuongelea masuala haya ya jumla na kinadharia katika warsha hizi, niliingia katika kutoa mifano ya matatizo ambazo makampuni yamekumbana nayo wakati wa kujaribu kupeleka shughuli zao katika nchi za mbali, kwenye utamaduni tofauti. Makampuni ya Marekani, kwa mfano, yamewahi kupata matatizo katika nchi za Ulaya na Asia. Hata namna ya kutangaza biashara inaweza kuwa chanzo cha matatizo. Tangazo ambalo linavutia wateja katika utamaduni fulani linaweza kuwa kero kwa watu wa utamaduni tofauti. Hata rangi zinazotumika katika tangazo zinaweza kuwa na maana tofauti au kuleta hisia tofauti katika tamaduni mbali mbali.

Kwa bahati nzuri, washiriki wa warsha hizi wamevutiwa na wamesisitiza kuwa ni muhimu warsha hizi ziendelee siku za usoni, kwenye mashirika, vyuo, na taasisi mbali mbali. Kwa upande wangu, nimefurahi kupata fursa ya kuongea kwa undani na waTanzania ambao tulikuwa hatufahamiani. Nimefurahi kuanza kuamsha fikra za masuala haya muhimu miongoni mwa waTanzania. Nimefurahi kuanza kujenga mtandao wa watu ambao tutaweza kuchangia kwa namna fulani maendeleo katika jamii yetu.

Katika kuthibitisha zaidi hoja hizi, nimekuwa nikiongelea mifano hai ya jinsi utamaduni wa Mmarekani unavyotofautiana na utamaduni wa Mwafrika, kama nilivyojionea mimi mwenyewe katika kuishi kwangu na waMarekani. Katika kufanya hivyo, nimekuwa nikitumia kitabu ambacho nimeandika, na ambacho kinatumika na waMarekani wanaofika Afrika, na pia waAfrika wanaoishi Marekani. Ninaandika muda wote, na hii ni njia ya kuendelea kujifunza mimi mwenyewe na kuendelea kutoa mchango wangu katika masuala haya muhimu.

Kitu kimoja ambacho nimekuwa nikisisitiza ni kuwa hili ni suala la elimu, na elimu haina mwisho. Tunawajibika kuanza kujielimisha na kuendelea hivyo bila kuchoka. Warsha moja au mbili haitoshi, bali ni mwanzo. Ni mwanzo mzuri, na nangojea kuendelea kuendesha warsha hizi siku zijazo. Zaidi Hapa kwetu

9 comments:

Anonymous said...

Labda tatizo kubwa lilikuwa nini maana halisi ya neno utandawazi, kwani sisi tulichukulia kuwa ni `mambo ya kisasa na tekinolojia yke' hasa katika mambo ya mitandao nk.
Kwa maelezo yako haya tumeelewa na ahsante kwa hayo

emu-three said...

Labda tatizo kubwa lilikuwa nini maana halisi ya neno utandawazi, kwani sisi tulichukulia kuwa ni `mambo ya kisasa na tekinolojia yke' hasa katika mambo ya mitandao nk.
Kwa maelezo yako haya tumeelewa na ahsante kwa hayo

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

utandawazi-WIZI...duh!

Tunazalisha tusichokula na tunakula tusichozalisha!!!!

Anonymous said...

sasa umeenda kuwafundisha watu jinsi ya kuishi na wamerekani?
hivi nani anakulipa kwa kazi hiyo?
kama hizo hela za bure zipo nipeni dili na mimi nikawafundishe wapemba jinsi ya kuishi na wamasaai.

Mbele said...

Ndugu unayeuliza kama ninawafundisha watu namna ya kuishi na wa-Marekani umegusia sehemu ndogo tu ya makala yangu. Wao wenyewe waliniomba niende. Sikujipeleka huko. Na huu ndio msimamo wangu. Niko tayari kumgundisha yeyote anayehitaji na anaonyesha hamu ya kujifunza kutoka kwangu.

Jambo la msingi ambalo nimelitaja na kulirudia katika makala yangu hapa juu ni wajibu wetu wa kujielimisha kuhusu tamaduni mbali mbali katika huu utandawazi.

Hii ya wa-Marekani nimeiingiza hapa kama mfano tu, kwa sababu hapo ndipo penye uzoefu wangu.

Mimi ni mwalimu. Wajibu wangu ni kuwaeleza wengine yale ninayoyajua, hata bila malipo. Sifanyi biashara. Kama watu wana chochote cha kunilipa, napokea. Kama hawana, siachi kuwafundisha. Kila mtu anayenijua, hata huku Marekani, anaelewa hivyo.

Mwaka huu, kwa mfano, nilikuja Tanzania, nikatumia laki nyingi katika kuzunguka sehemu kama Arusha, Tanga kwa lengo la kuendesha warsha, ili kuwaeleza watu yale ninayoyajua, ambayo pia nawaeleza wa-Marekani.

Sikuja kwa lengo la warsha tu. Nililipa shilingi laki tatu pale Diamond Jubilee Hall, ili kupata banda kwenye maonesho. Sikuchuma hela, bali ni mimi ndio nililipa, na kuwapa watu elimu ya bure. Soma hapa na hapa.

Mimi naiheshimu sana kazi yangu ya ualimu, na naiheshimu sana elimu, wala sipendezwi ninapoona watu wanaigeuza kuwa biashara. Mwalimu Nyerere alitufundisha vizuri kuhusu hilo, pale aliposema elimu ni haki ya kila binadamu, na kuwa haina mwisho. Alisema tujitafutie elimu maisha yetu yote.

Leo hii katika huu utandawazi wa kibepari, tumemsaliti Mwalimu na sasa hata elimu imekuwa biashara. Na kwa kweli, hii haiwezi tena kuwa elimu haswa, ingawa tunaiita elimu.

Makala yangu inazingatia utandawazi. Tofauti za utamaduni wa Mngoni, Mtumbatu, na Mhaya hazinisumbui, kwani kwa upeo huu wa utandawazi, utaona kuwa Mkuria na Mngoni wanafanana sana. Ukitaka kuelewa vizuri mawazo yangu kuhusu kipengele hiki, na ushahidi ninaotoa, soma kitabu changu kuhusu Wamarekani na Waafrika.

ADELA KAVISHE said...

asante kipenzi,,nimekubali nimeipenda sana,,juhudi zaidi elimu ndio ngao yetu

Mbele said...

Samahani wadau. Hapo juu nimechangia maoni, nikataja maonesho ya Diamond Jubilee Hall, katika para ya nne kutoka chini, ila kiungo kimojawapo hakifunguki, kwa vile sikukiweka ipasavyo. Samahani, ni hiki hapa.

MARKUS MPANGALA said...

Nimeandika na naendelea kuhubiri juu ya UTANDAWAZI NA UTAMADUNI. Nimeandika mengi kuhusu suala hili nafikiri Prof. Mbele umeendelea kunipanua zaidi. Kwa wale wanaoweza kuosma makala zangu katika gazeti la la serikali la HABARI LEO nimeandika kwa kirefu haya mambo. Na natarajia kuandika tena baada ya kutoka katika maonyesho ya sanaa mjini Bagamoyo. nimefanya mazungumzo na watu mbalimbali na aliyenivutia ni Ado Iko, mwana mama kutoka Japan aliyehudhuria tamsha hilo. Pia Julia Salmi ambaye ni mwafunzi wa chuo cha sanaa pale Bagamoyo. kw kweli tumelala, na bado tunahubiri serikali ituamshe. yawezekana lakini kwa hakika tunajifute vumbi kama tunazo na tuondoke sasa. Mimi najikita katika mahusiano ya binadamu katika tamaduni zao na teknolojia mbalimbali. nadhani hili ni eneo moja. najua mengine ni biashara,siasa na kadhalika

Mbele said...

Ndugu Mpangala, shukrani kwa mchango wako. Shukrani kwa kuweka taarifa kwenye blogu yako kuhusu maonesho ya sanaa Bagamoyo. Ni taarifa ile ndio ilinigutua, maana sikuwa nimejua habari hiyo.

Kuhusu masuala ya utamaduni na utandawazi, hapa Bagamoyo kuna dada ambaye anauza kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Namba yake ya simu ni 0754 445 956